Pare - Kilimanjaro

Local Knowledge & Climate Change Adaptation Project (LKCCAP)

Karibuni katika tovuti ya LKCCAP!

LKCCAP ni mradi wa utafiti wa kimataifa unaoshirikisha watafiti kutoka Marekani na Tanzania. Lengo kuu la utafiti huu ni kuchunguza kwa kina mienendo inayohusu uhusiano kati ya mazingira na shughuli za binadamu kuhusiana na ujihimilishaji na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi za jumuiya  ambapo miteremko manne kaskazini mwa Tanzania yameteuliwa kwa utafiti wa kina. Lengo pana la mradi  huu ni kupata ufahamu wa kina kuhusu mahusiano makuu kati ya mifumo ya maarifa-enyeji  na uwezo wa kujihimilisha na mabadiliko ya tabianchi katika muktadha wa mabadiliko ya kiasasi  sehemu za vijijini ambayo yanaweza  kuboresha au kuzorotesha michakato ya ujihimilishaji. Utafiti huu umeegemea katika data zilizopo tayari na data mpya kutoka kanda za milimani hadi kanda za nchi nusu-yabisi za kaskazini mwa Tanzania. Mbinu za utafiti huu zinajumuisha utafiti wa kina wa uwandani na utengenezaji wa mfumo shirikishi wa taarifa za kijiografia  ukiambatishwa na nyenzo za mitandao ya kompyuta pamoja na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (teknohama) ambazo zitawezesha matumizi yake kwa ajili ya shughuli za kubuni na kuunda  mandhari-dhahania na mitaala.

Timu ya watafiti wa LKCCAP inajumuisha nyanja mbalimbali na wataalamu kutoka nyanja kama vile jiografia ya maendeleo, menejimenti ya maafa, uchumi, ekolojia, isimu utamaduni, sayansi ya taarifa za kijiografia na sayansi ya tabianchi. Taasisi na asasi zinazoshiriki katika LKCCAP ni pamoja na Chuo Kikuu cha Ohio (Marekani), Chuo Kikuu cha Sokoine (Tanzania), Kituo cha Nishati, Mazingira, Sayansi na Teknolojia (Tanzania) na Chuo Kikuu cha Michigan State (Marekani).