Kiunzi cha Dhana
Uwezo wa Ujihimilishaji wa Kijiografia-jamii

Uwezo wa Ujihimilishaji

Uwezo wa ujihimilishaji ni uwezo wa mfumo kuelekeza kwa ufanisi mabadiliko yanayokuja polepole na kuibuka kwa kiasi kidogokidogo, ijapopokuwa mabadiliko ya muda mrefu kama haya huwa aghalabu yanashadidiwa na matukio makali ambayo huhitaji mbinu mahususi na za muda mfupi ili kuweza kukabiliana nayo. Katika ngazi za jamii ndogo ndogo, uchambuzi wa nyuma kuhusu uwezo wa ujihimilishaji umeegemea zaidi mkabala unaozingatia vipengele vya riziki endelevu ukijumuisha vipengele anuai vilivyofungamana vya mfumo wa kimazingira na shughuli za binadamu, kama vile mtaji wa kijamii, kibinadamu, kifedha, kimaumbile, na kiasili. Upungufu uliomo katika mikabala ya aina hii kuhusu ujihimilishaji na mabadiliko ya tabianchi ni kwamba wakati riziki za kaya zinazingatiwa kama kitovu (locus) cha vitu vyote viwili - athari na ujihimilishaji, uchanganuzi wake umefungwa katika mtizamo finyu unaozingatia tu tabia za juu juu na tabia za kiuchumi na teknolojia ya kilimo za kaya. Mtazamo finyu juu ya utajiri wa kiuchumi wa kaya (k.v., mtaji wa kifedha) na maarifa ya kiteknolojia (k.m., kijenzi kimojawapo cha mtaji wa kibinadamu) unafumbia macho dhima kuu  za mtaji wa kijamii na ushirikiano,  vitu ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa uwepo ama michakato ya ujihimilishaji na kutegemeana baina ya kaya, jumuiya, na asasi. Ujumuishaji wa asasi rasmi na zisizokuwa rasmi katika utafiti kuhusu ujihimilishaji na mabadiliko ya tabianchi ni mojawapo ya malengo ya msingi ya utafititi wetu shirikishi.


Uwezo wa Ujihimilishaji wa Kijiografia-jamii

Uwezo wa Ujihimilishaji wa Kijiografia-jamii unaweka msisitizo katika kutegemeana kwa mienendo ya ujihimilishaji kati ya makundi ya tabaka za kiuchumi na kitamaduni na katika miktadha yote ya kimazingira na kiasasi. Uchunguzi wetu kuhusu uwezo wa ujihimilishaji wa kijiografia-jamii unategemea viwango na kuzingatia ujihimilishaji  kwa hali iliyopo na hali inayoweza kutokea hapo baadaye kwa kuangalia haya yafuatayo:

  • Mitazamo ya watu kuhusu mabadiliko ya hivi karibuni katika ubadilikaji  wa kitabianchi na matarajio ya mabadiliko ya tabianchi katika siku za usoni;
  • Mikakati ya siku za nyuma na za sasa ya kukabiliana na kusimamia ubadilikaji, kama vile ukadiriaji wa mwelekeo, aina, na kiwango cha ujihimilishaji uliochochewa na tabianchi katika siku za usoni.
  • Muingiliano kati ya maarifa-enyeji na asasi za jumuia katika kujenga ama kuelekeza jinsi mtu au kikundi cha watu kinavyopokea mabadiliko katika ubadilikaji wa kitabianchi; na
  • Utabiri wa tabianchi kiukanda ambao unaruhusu kufanyika tathmini ya ugumu wa maisha utokanao na tabianchi ambayo inachangia katika kubuni na kuunda mandhari-dhahania ya ujihimilishaji katika ngazi ya jumuia na  ya kanda.