Kiunzi cha Dhana
Dhima ya Maarifa-enyeji

Maarifa-enyeji kuhusiana na Uwezo wa Ujihimilishaji wa Kijiografia-jamii

Maarifa-enyeji yanaendelea kutambuliwa kama kitovu katika mienendo  ya ujihimilishaji unaotokana na mabadiliko ya tabianchi, lakini ni watafiti wachache ambao wamejumuisha suala la maarifa-enyeji katika viunzi vyao vya ujihimilishaji au katika utafiti wa uwandani uliolenga taarifa/data kuntu. Wala hawajajibidiisha kufikiria tabia ya maarifa-enyeji ya kuwa na umbo-changamano  na kubadilikabadilika kufuatana na mazingira (dynamic). Idadi kubwa ya tafiti zihusuzo mabadiliko ya tabianchi imelenga zaidi katika mikakati ya ujihimilishaji katika ngazi za kanda na taifa wakati ujihilimishaji katika ngazi ya chini pamoja na maarifa-enyeji ambapo ujihimilishaji huo umeegemea havijapewa uzito unaostahiki katika uwanja huu. Pia kitu kingine muhimu kinachokosekana ni  ujenzi wa nadharia  juu ya matatizo na fursa za kuunganisha kikamilifu kwa kuzingatia utaalamu suala la maarifa-enyeji katika mjadala (discourse) wa sera na mipango ya miradi.

Mbali na idadi kubwa ya vijenzi vyake changamano (composite domains) na mwingiliano wavyo na kutegemeana kusikoepukika, pia kuna tabia nyingine muhimu za maarifa-enyeji. Kwanza, maarifa-enyeji sio kitu cha aina moja (monolithic), bali ni kitu kilichojengwa kwa vijenzi anuai, kwa namna mabalimbali, na hutofautishwa kwa namna ambazo aghalabu huzaa utaalamu unaotambuliwa katika ngazi hiyo ya jumuiya au jamii ndogo husika. Pili, wakati inawezekana kabisa kuwepo maneno na misemo ya uyaeleza katika jumuiya husika, maarifa-enyeji hayo sio lazima kuwa kitu kinachotamkwa au kusemwa hadharani – yaani kitu ambacho kinatambuliwa mahususi kuwa maarifa-enyeji, kijadiliwe, kidahaliwe (debated), au kitatanishwe (problematized). Katika maisha ya kila siku maarifa-enyeji yanaweza kuwa ni kitu kisichotambulika kwa uwazi na kinachofanyika kimyakimya bila wahusika kukitambua na kukieleza kwa uwazi (tacit) lakini wanajumuiya au wanajamii wanajifunza na kupata maarifa hayo kwa kuwa sehemu ya uhusiano wa kikoo au mahusioano mengine ya kijamii katika jamii husika. Tatu, maarifa-enyeji sio kitu kilichojitenga au kutengwa kutoka maarifa na athari za nje ya jamii husika.

Vipengele vya maarifa ya utaalamu kutoka nje vilivyojikita katika mazingira ya asasi za ngazi ya jumuiya vinaweza kubainishwa, kuteuliwa, na kushirikishwa na hata kurekebishwa ili vikidhi mahitaji ya ngazi hiyo husika. Suala jingine linalohusu upenyezo huu na athari za kutoka nje ni uwezekano kwamba mabadiliko ya kimazingira au uhamishwaji utokanao na shughuli za maendeleo unaweza kupelekea kuwepo kwa mandhari tofauti kabisa ya kisura na kibaolojia na hivyo kufanya maarifa-enyeji ya awali kuonekana kukosa ufanisi.  Kiunzi-dhana cha mradi huu wa utafiti kinabashiri kuwepo kwa mwingiliano tata kati ya mifumo ya maarifa ya kienyeji na utaalamu kutoka nje ambao unaathiri uwezo wa ujihimilishaji kijiografia-jamii.