Athari Pana
Jumuiya, Sera, & Ukuzaji wa Mitaala

Umuhimu wa kisera, kielimu, na kisayansi wa utafiti huu umeshonana na kuwa kama kitu kimoja kwa sababu ya udau mseto na mkabala shirikishi wa mradi huu wa LKCCAP. Changamoto ambazo hazijawahi kutokea kuhusiana na riziki za kaya za vijijini na kuhusiana na sera za dola ambazo zinasababishwa na mabadiliko ya tabianchi zitaongeza umuhimu katika uchambuzi ambao tutaufanya kwa kujikita katika mada ya jumla ya maarifa-enyeji, kustahamili, na kujihimilisha.

Mtazamo wa jumuiya kuhusu ujihimilishaji

Athari za mradi huu kwa jumuiya ni pamoja na mchango wa moja kwa moja katika kubuni na kutengeneza mipango ya ujihimilishaji unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya jumuiya hususani katika maeneo ya vijijini katika nchi zinazoendelea kwa kukuza mbinu ya utafiti inayobaini maarifa-enyeji muafaka na dhima ya asasi za ngazi ya jumuiya katika maendeleo yake. Hili litatoa taarifa muhimu juu ya asasi za kijumuiya, tarifa za mabadiliko ya tabianchi, maarifa-enyeji na michakato ya ujihimilishaji. Hali ya ushirikishi na taarifa zinazoonekana katika maumbo za mbinu ya utafiti inaboresha ufanisi wake unaotarajiwa. Uundaji na tathmini ya mbinu ya utafiti ni kitu endelevu kwa maana kwamba kitaendelea kufanyika katika kipindi chote cha mradi huu, na hatimaye kujadiliwa katika warsha za wadau katika ngazi ya jumuiya.


Umuhimu wa Kisera

Tunaangalia sehemu mbalimbali za jamii ambamo utafiti huu utanufaisha sera za ujihimilishi uliochochewa na mabadiliko ya tabianchi zinazotungwa na asasi za kijumuiya, kitaifa, na kimataifa. Hususani, utafiti huu utawasaidia watunga sera wa bara la Afrika kwa kuingiza michakato ya ngazi za kijumuiya katika sera za kitaifa za ujihimilishaji unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi. Tutabadilishana matokeo ya utafiti uliopendekezwa na kitengo cha kitaifa cha Tanzania kinachohusika na uratibu wa maafa (Tanzania National Disaster Management Division) na tutawasilisha mihutasari ya sera kutoka katika utafiti kwa kamati ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na kamati ya mikakati ya kupunguza umaskini (Poverty Reduction Strategy Paper – PRSP) iliyo chini ya Wizara ya Mipango, Ofisi ya Rais ili kutoa ushauri wa kujumuisha masuala ya ujihimilishaji utokanao na mabadiliko ya tabianchi katika PRSP. Katika ngazi ya kimtaifa, matokeo ya utafiti huu na kiunzi na mbinu za utafiti zilizotumika zitaboresha kazi za kisayansi katika sehemu nyingine duniani wakati ambapo mchakato wa mpito utakapokuwa umeanza kuelekea kuundwa kwa kiunzi kipya cha sera ya kimataifa kuhusu ujihimilishaji utokanao na mabadiliko ya tabianchi.


Mtaji wa Kielimu

Shughuli za mradi huu zinayo manufaa kielimu kwa njia mbalimbali. Uundaji wa zana za kimtandao wa kompyuta za ufananishi na ufundishaji utakuwa ni mchango mkubwa katika elimu ya kijiografia inayohusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ujihimilishaji utokanao na hali hiyo. Zana hii itaingizwa na kufungamanishwa katika mitaala ya sasa ya Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Ohio (OU), na Chuo Kikuu cha Michigan State (MSU). Shughuli za kielimu nchini Tanzania zitalenga katika ukuzaji wa vifaa vya kimtaala ambavyo vitafanyiwa majaribio na kutumika katika vyuo vya SUA na UDSM, ambapo matokeo ya utafiti huu juu ya atahri za mabadiliko ya tabianchi na ujihimilishaji yatachangia katika ukuzaji wa mitaala ya masomo ya Baolojia, Usimamizi wa Maliasili, na programu za maendeleo vijijini. Mtaala ambao utatokana na mradi huu wa utafiti pia unatarajiwa kuboresha mafunzo ya watumishi wa umma wa siku za usoni katika wizara za serikali kama vile misitu, mazingira, na kilimo. Katika ngazi ya elimu ya sekondari, timu ya utafiti huu imejizatiti ipasavyo kuhakikisha taarifa mpya zinazohusu athari za mabadiliko ya tabianchi na ujihimilishaji utokanao na mabadiliko hayo zinachangia katika uboreshaji wa mitaala ya shule na mafunzo ya ualimu. Vitengo vya mradi na ufundishaji wa kimtandao pia vitarutubisha ufundishaji wa wanafunzi wanaofanya masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo vikuu vya Marekani vinavyoshiriki katika mradi huu, ambapo mbinu za utafiti na matokeo yake zitachangia kuboresha kozi katika GIS, Katografia, jiografia ya Afrika, na Masuala ya Wanawake na Mazingira. Vifaa vitokanavyo na utafiti na mbinu zake pia vitasambazwa kama vifaa vya kisayansi, makala za mradi, maelezo mafupi ya kisera, pamoja na toleo la PGIS kutundikwa kwenye tovuti ya mradi huu wa LKCCAP.